Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Dkt. Zakia Mohammed Abubakar amewanasihi wanafunzi wapya kutumia muda wao wakiwa Chuoni kwa kusoma kwa bidii na kupuuza mambo mengine yasiyo ya msingi ili kujijengea uwezo wao kimasomo ili hatimaye waweze kulisaidia taifa katika hali ya uweledi na kujiamini. Nasaha hizo zimetolewa katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Kampasi ya Tunguu tarehe 16 Novemba, 2020 wakati akiwakaribisha wanafunzi hao wanaojiunga na Chuo kwa kozi na ngazi mbali mbali kwa mwaka wa masomo wa 2020/2021.

Makamu Mkuu wa Chuo aliwapongeza wanafunzi hao kwa kupata fursa ya kujiunga na Chuo Kikuu kwani alisema ni asilimia tatu (3%) tu ya wanafunzi wanaoanza skuli za msingi ndio hubahatika kupata fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwa ngazi ya Chuo Kikuu hivyo ni vyema wakatumia busara ya kuitumia fursa hiyo kikamilifu. Alifafanua kuwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kipo kwa mujibu wa sheria na kinatambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), aidha alisema kuwa kwa sasa Chuo kina mahusiano na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu zaidi ya 70 duniani kote hivyo ni vyema kwa wanafunzi pia kutumia fursa za mahusiano hayo kwa kusoma kwa bidii ili kuendana na wakati uliopo.

Sambamba na ufafanuzi huo, Dkt. Zakia amewahakikishia wanafunzi kupata mashirikiano ya juu ya kitaaluma kutoka kwa Uongozi wa Chuo ambao uko karibu mno kimashirikiano na Serikali ya Wanafunzi ya Chuo (SUZASA) kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanasoma wakiwa na amani ya hali ya juu. Aidha aliwatakia kila la kheri wanafunzi wote waliomaliza masomo yao Chuoni hapa.  Kwa upande wake Dkt. Ali Makame Ussi, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri aliwataka wanafunzi hao kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo ili kupata taaluma itakayowawezesha kusogeza harakati za kimaendeleo katika jamii na taifa kwa jumla.

Aidha aliwataka wanafunzi hao kufuata taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya  SUZA ili kuepusha usumbufu wowote unaoweza kutokea sambamba na kusisitiza kuongeza bidii katika masomo kwani jamii zina matumaini makubwa juu yao. Dkt. Ali Ussi alieleza kuwa ili Chuo kitekeleze majukumu yake ya kitaaluma ipasavyo ni lazima sana kwa wanafunzi wote kutekeleza wajibu wao wa kulipa ada zote zinazohusika kwa wakati, hivyo hakutakuwa na sababu yoyote itakayokubaliwa kwa mwanafunzi kuacha kutekeleza wajibu huo na kwamba uongozi wa Chuo kwa upande wake utafuatilia jukumu hilo la wanafunzi kwa karibu sana. Alitoa msisitizo kwa wanafunzi kuepukana na usumbufu usio wa lazima kwa kuacha kulipa ada na stahiki nyinginezo.

Jumla ya wanafunzi 2597 wamedahiliwa katika fani mbali mbali za masomo katika Shahada ya Uzamivu, Shahada za Uzamili, Shahada za Kwanza, Stashahada na vyeti katika mwaka wa masomo wa 2020/2021 unaoanza rasmi tarehe 23 Novemba, 2020.