SUZA YAPONGEZWA KWA KUANDAA MPANGO WA MATUMIZI YA ARDI YA CHUO

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhe. Dk. Khalid Salum Mohamed, ameupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kwa kuandaa mpango kabambe wa matumizi ya ardhi. Aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa kupitia mpango kabambe wa matumizi ya ardhi ya Chuo kwa miaka ishirini (20) ijayo kuanzia 2023-20243.

Waziri Khalid amesema ameridhishwa na mpango kabambe wa matumizi ya ardhi ya Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wenye lengo la kuimarisha miundombinu ya Chuo ikiwemo majengo na barabara. Alisema, ni vyema mpango huo kupelekwa serikalini ili hatua za utekelezaji ziweze kuchukuliwa kwa kushirikiana na wadau na kuwataka Wizara na Taasisi zingine kuiga mfano wa SUZA kwa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi.

Aidha, Dk. Khalid, alisema amefurahishwa zaidi na mashirikiano waliyoaanzisha kwani sio jambo linalofanyika mara nyingi kwa vyuo vikuu kuwa na mashirikiano ya karibu namna hiyo. Hivyo, alisema Chuo cha SUZA, kimekuwa na mashirikiano makubwa na mazingira yatakayowezesha kuendelea na mashirikiano na vyuo vyengine vya ndani ja nje ya nchi.

Akitoa maelezo kuhusu mpango kabambe huo, Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Moh’d Makame Haji, alisema, chuo kimekuwa na muelekeo wa mabadiliko makubwa ya kuwa na majengo ya kisasa na mazingira mazuri ya kusomea kwa wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho. Alisema uongozi wa Chuo umeona ipo haja kwa sasa kutumia eneo hilo ili kufikia adhma na malengo waliyojipangiwa kwa mujibu wa matakwa na mahitaji ya ya chuo.

Akifafanua zaidi alisema, kazi ya kuandaa mpango kabambe huo imeanza Machi 6 mwaka huu na hivi sasa ipo katika hatua ya mwisho ya kukusanya maoni ya wadau na kukamilika. Aidha, alieleza kwa kusema kuwa kamati ya wataalamu imeonesha nia ya kuona mpango huo unafanikiwa ili kuleta maendeleo ya nchi kwa ujumla yake. Alisema mpango huo ni kuwa na chuo chenye hadhi, maendeleo na mabadiliko ya kuona kinafanya kazi ya kusaidia maendeleo ya nchi na muonekano wa chuo chenyewe.

Sambamba na hayo, amefahamisha kuwa mpango huo uliowashirikisha wataalamu kutoka chuo kikuu cha Ardhi (ARU) utafanyika ndani ya miaka 20 kuanzia 2023 hadi 2043 na utekelezaji wake umegawanywa kwenye awamu tatu ambapo zaidi ya majengo 35 yanatarajiwa kujengwa yakiwemo majengo ya Skuli zote zilizo chini ya SUZA, Maabara ya Sayansi na dakhalia za wanafunzi, Skuli ya Elimu, Jengo la utawala, mkahawa wa wanafunzi, viwanja vya michezo, na nyumba za walimu.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Sabiha Filfil Thani, alisema, kamati imefurahishwa sana mpango huo kapambe ambao umebainisha na kuweka bayana maeneo yote muhimu.

Hivyo, aliwaomba uongozi wa SUZA kujipanga kwa kuwa uboreshwaji wa majengo unaendelea na kuhakikisha  walimu wenye utaalamu wanakuwepo katika chuo hicho ili wanafunzi waweze kuwa na taaluma iliyokuwa bora na kuondokana na kutupa fedha nyingi kwa ajili ya kuchukua wataalamu kutoka nje.

Akiwasilisha mpango kabambe wa chuo Mhadhiri Mwandamizi Dkt. Fredrick Bwire Magina, kutoka chuo Kikuu cha Ardhi alisema, mpango huo umezingatia hali halisi ya maendeleo ya Chuo na aliahidi kutekeleza mpango huo kwa mujibu wa makubalino yaliyopo ili lengo liweze kutimia.

Mkutano huo wa wadau wa kupitia mpango kabambe wa matumizi ya Ardhi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar ulifanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Utalii Maruhubi na kuhudhuriwa na Wakurugenzi na maafisa kutoka kwenye Wizara na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na viongozi, wafanyakazi na wawakilishi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo.