Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimesema kitaendelea kuunga mkono jitihada za serikali ikiwemo kushirikiana katika utoaji wa huduma zilizokuwa bora kwa wananchi.

Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Prof. Moh’d Makame Haji, alisema hayo alipokuwa akizungumza katika bonanza la utoaji wa huduma za Afya katika kituo cha Sebleni, liloandaliwa na skuli ya Afya na Sayansi za tiba (SUZA).

Alisema, Bonanza hilo ni muendelezo wa kazi wanazozifanya katika Chuo hicho ikiwa na lengo la kuona wananchi wanakuwa na afya bora.

Alisema huduma hizo wanazitoa kwa ushirikiano mkubwa na Wizara ya Afya fya kupitia madaktari wao ikiwa na lengo la kutekeleza mikakati ya serikali katika kuhakikisha afya za wananchi zinaimarika na kuweza kutumika katika ujenzi wa taifa.

“Serikali kuu imedhamiria kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa hospitali, kufundisha wataalamu mbalimbali na sisi kama Chuo Kikuu cha Taifa tunajukumu hilo la kuunga mkono juhudi hizi zinazoendelea ili tuwe tunaenda sambamba na malengo ya serikali” alisema.

Hivyo, alisema Chuo kimekuwa kikifanya shughuli mbalimbali na tafiti za kusaidia jamii ikiwemo utoaji wa taaluma mbalimbali, kushirikiana na jamii kwa fani zilizopo ili kuondosha changamoto zinazoikabili jamii.

Sambamba na hayo, alifahamisha kuwa katika bonanza hilo, watatoa huduma mbalimbali ikiwemo utumiaji sahihi wa dawa ushauri kwa mama wajawazito na watoto, pamoja na magonjwa mbalimbali yanayowasumbuka wananchi watakaofika katika bonanza hilo.

Nae, Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba (SUZA), Dkt. Salma Abdi Mahmoud, alisema, lengo ni kuona wananchi hao wanapatiwa huduma iliyokuwa bora na watumiaji ni wengi.

Alisema, katika utafiti wameona kuna kesi mbalimbali na ndio wakaona ni vyema wakenda kutoa huduma katika kituo hicho na wamekuwa na madaktari mbalimbali wakiwemo wataalamu bingwa wa kina mama na watoto na afya ya meno.

Sambamba na hayo, alisema lengo lao ni kuwafikia wananchi waliokuwa na changamoto mbalimbali za kiafya kwa kuwapa elimu ya afya na lishe bora na kuangalia kesi zilizokuwa haziwezi kufikiwa na wakizitambua watazipeleka rufaa mnazimmoja kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hivyo, aliwataka wananchi kujitokeza katika bonanza hilo ili kuweza kupata huduma za upimaji wa maradhi mbalimbali na kujua maradhi gani yanawakabili na kuweza kupatiwa huduma kabla hayazidi.

Nae, Daktari dhamana wa wilaya ya Mjini Dk. Ibrahim Makame, alisema wamefurahishwa na kuwepo kwa bonanza hilo kwani litasaidia kujua wananchi wanakabiliwa na maradhi gani katika wilaya yao.

Alisema, vipaumbele vya serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuimarisha afya ya msingi na wamefarajika kuona Chuo Kikuu cha Taifa Cha (SUZA)kulifanya hilo kwa vitendo na kuwapongeza kwani wameonesha kuunga mkono serikali yao.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi waliopatiwa huduma katika bonanza hilo, Sheha wa Shehia ya kwawazee, Abrahman Omar Kasongo, alisema wamefurahishwa na kupatiwa matibabu kwani wameweza kutambua maradhi mbalimbali yanayowasumbua na kuweza kupata tiba.