SUZA MWENYEJI WA KONGAMANO LA KADA YA UTABIBU AFRIKA MASHARIKI

Maafisa Tabibu Afrika wametakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kufikia malengo waloyokusudia pamoja na kuunda chombo maalum kitachowasaidia katika utendaji wao wa kazi. Kauli hiyo imetolewa na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe Othman Masoud Othman kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi wakati akifunguwa Kongamano la Kwanza la Kimataifa katika Ukanda wa Afrika Mashariki la Maafisa Tabibu lililofanyika Taasisi ya Utali ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Kampasi ya Maruhubi.

Mhe Othman amesema ni ”vyema kupitisha maazimio watakayowasaidia kwa pamoja katika kukuza na kuendeleza taaluma hiyo ili kuweza kutengeneza kada ya utabibu yenye kufahamika na yenye miongozo maalum itakayotambulika Afrika Mashariki, kwani taaluma hiyo bado ipo nyuma katika masuala mbali mbali yakiwemo maslahi, sheria pamoja na uboreshwaji wa kiutendaji hususani nchini Tanzania.

Kwa upande wake Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Profesa Moh’d Makame Haji amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujadili na kuibua wazo la kuweka mfumo sahihi wa kutengeneza kada ya afisa tabibu utakaotambulika kwenye ukanda wa Afrika. Prof. Moh’d amesema katika nchi za Afrika kada hiyo imekuwa na umuhimu na mchango mkubwa kwa kutoa huduma za afya.

Nae Rais wa Shirikisho la Matabibu wa Afrika (GACOPA) Austin Oduor Otieno amesema wanataka kuielezea jamii umuhimu wa Afisa Tabibu pamoja na kuweka chombo maalum ambacho kitawashirikisha Afrika mzima.

Kongamano hilo la siku mbili limeeandaliwa na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kwa kushirikiana na shirikisho linalosimamia matabibu Afrika Mashariki (GACOPA), ambapo zaidi wa wajumbe mia mbili kutoka nchi za Kenya, Ethiopia, Uganda, Rwanda, Burundi, Sidani ya Kusini, Botswana na Tanzania pamoja na wataalamu wa kada za utabibu kutoka Uingerrza wameshiriki.