KONGAMANO LA KITAALUMA LA MAADHIMISHO MIAKA 60 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR
Vyuo Vikuu vijikite kuichambua historia isipotoshwe-Prof. Nkenda
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Profesa Adolf Faustine Nkenda amesema vyuo vikuu vina jukumu la kuichambua historia kwa uwazi na kiuzalendo kwa kuzingatia kuwa haipotoshwi.
Hayo aliyasema wakati akifungua kongamano la kitaaluma likiwa ni sehemu ya shamra shamra za maadhimisho ya miaka sitini (60) ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
Profesa Nkenda alisema historia ni uwanja wa mapambano na inatoa fursa kwa watu kuchora picha mbali mbali.
Aliongeza kuwa Mapinduzi katika nchi yoyote duniani yanafanyika kwa lengo la kubadilisha mfumo na kama zilivyo nchi nyengine, Zanzibar imeitumia dhana hiyo kuleta usawa wa binadamu.
‘Tuna jukumu la kuiangalia kwa macho meupe, uhakika na ukweli tusije kusababisha vizazi vijavyo kuwa na tafasiri tafauti’, alisema.
Kongamano hilo linabeba kauli mbiu ‘Tuimarishe Uchumi, Uzalendo na Amani kwa Maendeleo ya Taifa Letu’, lilifanyika kwenye ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein uliopo Kampasi ya Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman, aliwahimiza kujifunza historia ya Zanzibar .
‘Muelewe historia ya nchi yenyu kwani skuli haisomeshwi kama inavyostahiki. Someni huu ndo wakati wenu,’ aliwakumbusha. Akizungumzia kuhusiana na maendeleo ya elimu Zanzibar, Mhe. Haroun alisema Chuo Cha Taifa cha SUZA kilianzishwa miaka 22 iliyopita kikiwa na wanafunzi 54 na sasa kina wanafunzi 7000.
Haroun aliongeza kuwa kabla ya Mapinduzi kama hujulikani huwezi kupata elimu na mwenye asili fulani anayeishi mjini ni tafauti na anayeishi shamba, hali ambayo kwa sasa ni tafauti.
Aidha, aliongeza kuwa makongamano kama haya yafanyike kwenye Wilaya za Unguja na Pemba ili nao wapate taaluma hii.
Akichangia mada kuhusiana na harakati za ukombozi Zanzibar na Afrika, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mhe. Steven Wasira alisema Mzee Karume alichukia dhulma na alipenda haki na ukichukia dhulma unachukua hatua.
Aliongeza kuwa Mzee Karume aliamini katika umoja na hivyo kuungana na viongozi wengine wa Afrika ili kupigania uhuru kwa pamoja.
‘Mapinduzi haikuwa ajali ilikuwa lazima yafanyike kwa njia ya amani yasingekuwa’, alisema.
‘ Historia huwezi kuibadilisha ukiibadilisha utaandika unavyotaka lakini historia itabaki pale pale’, Mhe. Wasira alisema.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), Khamis Abdallah, alisema miongoni mwa kazi za Chuo kikuu ni kuchechemua fikra ambapo leo wasomi na wabobesi wana fursa ya kujadili historia, maendeleo na mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 60 iliyopita.
Akichangia mada ya wasifu wa Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Ndg. Ali Shaaban ambaye ni msomi na mtunzi wa vitabu alisema, Mzee Karume alijenga misingi imara ya kuwaweka watu pamoja kwa kuondoa dhana ya kujiona bora hali ambayo inasababisha kuleta mfarakano.
Alifafanua kuwa nchi kadhaa zilikuwa na utawala wa jadi, kabila ama kundi la kidini lilijiona kuwa ni bora na hivyo kupambana na kundi jengine. Alitoa mfano ya taifa ya Israel ambapo tangu mwaka 1948 lilipoundwa hadi sasa wanaendeleza mgogoro na kuuwana.
‘Baada ya Mapinduzi Mzee Karume alifuta dhana ya kujiona kuwa mimi ni bora kwani ikifikia hapo huishia kuuana’, alisistiza
Mshiriki wa kongamano hilo, ambaye pia ni mwalimu wa somo la historia kampasi ya Tunguu Bi. Ziada Mussa, alisema kuwa amejifunza mambo mengi ambayo hakuwahi kuyasikia katika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, alipendekeza makongamano kama haya kuwa endelevu ili kuepusha kuharibiwa historia lakini pia kuwajenga vijana kizalendo.
Mshiriki mwengine wa mwaka wa kwanza kutoka Kampasi ya Tunguu huko Nkurumah, Ndg. Samuel Nathania, alisema hakuwahi kuifahamu historia ya Mapinduzi ya Zanzibar kwani yeye siyo mzaliwa wa Zanzibar, ila amevutiwa na mada zote zilizowasilishwa.
Aliongeza kuwa ameona faraja pia kongamano kuwashirikisha viongozi waliobobea katika masuala mbali mbali ya kitaaluma.
Kongamano hilo ambalo liliongozwa na Mwenyekiti, Balozi Mohammed Hamza, lilipambwa na utenzi wa papo kwa papo uliosomwa na Kassim Yussuf, lilihudhuriwa na wageni mbali mbali hilo akiwemo, Naibu Katibu mkuu Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, wakuu mbali mbali wa SUZA, wanafunzi na wanataaluma kutoka Chuo cha Alsumeit, Zanzibar University na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, chuo cha Sayansi na teknoliojia na Chuo Kikuu Huria na Chuo cha Kiislamu
Wengine ni wawakilishi wa Jumuia za vya siasa Tanzania, ACT, Ada -tadea Chadema, wazaazi, vijana, wanawake, na waandishi wa habari.