MAHAFALI YA 19 SUZA
Dkt. Samia aongeza kasi kuibua wanawake vinara
Na Mwandishi Wetu, SUZA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa jamii kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuongeza kasi ya ushawishi wa wanawake kujiunga katika fani mbali mbali za masomo.
Akizungumza katika sherehe za mahafali ya 19 katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, Dkt. Samia alisema hivi sasa wakati umebadilika na kwamba wanawake wamekuwa mstari wa mbele kujitafutia maendeleo yao na jamii.
Katika mahafali hayo wahitimu 2012 walitunukiwa vyeti ambapo miongoni mwao wahitimu 1229 ni wanawake.
‘Asilimia 58 ya wahitimu ni wanawake, haya ni matokeo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Wakati wetu wanawake kila tukienda juu (elimu ya juu) tunapungua leo imekuwa tafauti’, alisema kwa fahari.
Mazungumzo ya Dkt. Samia yaliafuatia na baada ya wasifu wake uliosomwa mbele ya hadhara ya wageni na viongozi mbali mbali waliokuwepo kwenye mahafali hayo kabla ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kumtunuku Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Utalii na Masoko kutokana na na mchango mkubwa alioutoa katika sekta ya utalii na maendeleo ya taifa.
Akizungumzia mchango wake katika maendeleo ya Zanzibar, Dkt. Samia alisema tunzo aliyopokea ni heshima kwa watanzania wote katika kutekekeleza majukumu yake.
Aliongeza kuwa katika kufanya kazi zake alishirikiana na wengi na aliwaita kubadilishana mawazo kazi zao walizofanya na kubaini kuwa walifanyya mambo mengi makubwa ya kuing’arisha nchi.
’ wakati tunafanya yote haya, hatukuwaza kama zile zitajulikana na kutunukiwa heshima kubwa’.
‘nilitolewa kichochoroni nikapewa Wizara inayoshughulikia masuala ya wanawake na watoto na baadaye Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji. Heshima hii ni kwa bosi wangu, Dkt Amani Karume, nashukuru kwa malezi uliyonipa na leo napata heshima kubwa’ alishukuru huku akimuangalia Dk. Karume.
Akitoa nasaha zake kwa wahitimu, Dkt. Samia aliwataka kwenda kwenye jamii na kuzikabili changamoto zilizoko kwenye jamii kwa mfumo hasi.
Aidha, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuridhishwa kwake na kuwepo idadi kubwa ya wahitimu wanawake wengi wanaofanya vizuri katika masomo yao.
‘nachukua fursa hii kukupongezeni tena wahitimu wetu hasa wanawake ambao kwa mara nyengine wametokea kuwa ndiyo wengi kuliko wanaume, wahitimu wanawake ndio wanaoshika nafasi nyingi za juu katika masomo mbali mbali.
Mapema Makamo Mkuu wa Chuo cha Taifa SUZA, Profesa Moh’d Makame Haji alisema Chuo kimeandaa programu mpya ya Ujasiriamali na ubunifu ambapo kati ya wahitimu 18 waliotunukiwa vyeti wahitimu 16 ni wanawake.
Katika hatua nyengine, chuo kimetoa wanafunzi bora ambao wote ni wanawake kwa kila ngazi kama vile Shahada ya Kwanza aliyetoka katika fani ya mazingira ni Rose R Kibiriti, Stashahada ni Farhia farhan Juma aliyehitimu katika fani ya kinywa na meno na aliyehitimu katika ngazi ya Cheti na Khadija Paquet fani ya TEHAMA.
Mwisho