Na Mwandshi Wetu, SUZA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Hussein Ali Mwinyi amekabidhi tunzo maalum kwa viongozi na wataalamu waliobuni fikra ya kuanzishwa  na kuimarishwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Tunzo hizo zimetolewa  kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu, Mhe. Jamal Kassim katika uzinduzi wa Mkusanyiko wa Kwanza wa Kitaaluma wa Chuo hicho (SUZA 1st Convocation) uliofanyika katika  Kampasi ya Chuo huko Maruhubi. Hafla hiyo  ilikuwa ni miongoni mwa shamra za maadhimisho miaka 60 ya Mapinduzi   ya Zanzibar ambayo kilele chake  kitafanyika tarehe 12 Januari mwaka   huu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mwinyi aliipongeza  SUZA kwa kukamilisha azma yao ya kuunda Convocation  na kuongeza kuwa convocation za vyuo zilizofanikiwa duniani zimeweza hata kuwa na vyanzo vya mapato imara vinavyoweza kusimamia na kushauri katika shughuli za maendeleo na kitaaluma za vyuo vinavyohusika.

”Kuanzisha Mkusanyiko wa Kitaaluma (convocation) ni jambo linalohitaji kujikubalisha kwa walengwa kutokana na ukweli kwamba convocation inasimama kama Taasisi yenye kamati za utendaji na usimamizi wa mipango yake ambayo inahitaji muda wa kutosha ili kufanikisha majukumu yake,”

Aidha, aliongeza kuwa hivi sasa dunia inapiga hatua za  maendeleo kwa kutumia wasomi zaidi katika kufanikisha utayarishaji na utekelezaji wa sera na mipango ya kimaendeleo ya nchi mbalimbali,  hivyo, ana matumaini kuwa wanataaluma na wana alumni wote waliopita kwenye mikono ya Chuo hiki wataitumia vizuri fursa hii ya Mikusanyiko ya kitaaluma kwa kuleta mabadiliko chanya kwa jamii ya SUZA na Zanzibar kwa ujumla.

Chuo cha SUZA kimeundwa miaka 22 iliyopita ambapo chimbuko la kuundwa kwake limetokana na fikra  za Mhe. Alhaj Dkt. Salmin Amour Juma,  Rais Mstaafu wa  Awamu 6 ya  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  wakati huo akiwa Dkt. Mohammed Gharib  Bilal, Waziri wa Kiongozi  ambao kwa pamoja SUZA inautambua mchango wao ulioifikisha Zanzibar kuwa kitovu cha kuzalisha wasomi na wataalamu kwenye fani mbalimbali.

Aidha, Mhe. Alhaj Dkt. Amani Abeid Karume  Rais Mstaafu wa awamu ya 7 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  naye ameonesha jitihada kubwa za kukiimairisha chuo hiki sambamba na Mhe. Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  ambaye pia ni  Mkuu wa Chuo wa kwanza kuanzisha mkusanyiko wa kitaaluma “Convocation” wa SUZA.

Hali kadhalika,  mawaziri vinara wa Elimu na Mafunzo ya Amali  Zanzibar  katika vipindi tafauti waliosimamia kuikuza fikra ya Dkt. Salmin ni Mhe. Haroun Ali Suleiman, Mhe. Omar Ramadhan Mapuri Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee  wakati huo akiwa Katibu Mkuu katika Wizara hiyo kwa kipindi kirefu  alisimamia Kamati za Uratibu wa Uanzishwaji wa  SUZA.

Vile vile, SUZA inatambua  michango  ya  wanakamati   akiwemo Prof. Saleh Idris Muhammed   Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya SUZA na  Dkt. Said Gharib Bilal akiwa Katibu wa Kamati Tendaji hiyo. Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Dkt. Bishara Theneyan Mohamed, Dkt. Ibrahim Said Rashid Msabaha, Marehemu Bw. Ahmed Mohammed Abdulrahman, Prof. Abdul Sheriff, Prof. Ali Seif Mshimba, Marehemu Prof. Haroub Miraji Othman na Prof. Geoffrey Rafael Vehaeli Mmari.

Aidha, tunzo  nyengine maalum imetolewa kwa Bw. Said Salim Bakhresa

kwa kutambua mchango wake kwa jamii ya SUZA katika harakati za awali za uimarishaji wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.

Katika upangaji safu wa kukiendeleza chuo hicho, mchango wa  wajumbe wa sekretariet ya uanzishwaji wa  Chuo hicho  pia inathaminiwa  kama vile Bi. Maimuna Rashid Shaaban, Bw. Waadili P. L. Kavishe, Bi. Rabiya Tajiri Ali   ambao pia wamenukiwa tunzo za heshima.

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Profesa Mohammed Makame Haji, alisema kuwa Mkusanyiko wa kitaaluma katika unalenga kuchochea mabadiliko na maendeleo kwa ujumla. Miongoni mwa malengo  hayo ni kuimarisha na kukuza ushirikiano baina ya wadau mbali mbali SUZA; kuimarisha ustawi, hadhi, ubora na maendeleo ya Chuo; kuwakutanisha wadau wa Chuo, kujadili na kushauri mambo mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Chuo hiki.

Uongozi wa SUZA  na wafanyakazi wote  unawapongeza kwa mbegu bora walizozipanda zinazoendelea kutoa mavuno mazuri ya kujivunia.