Dk. Karume aridhia kuwa Balozi Kigoda cha Karume
Na Mwandishi Wetu
Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, amepokea ombi la kuwa Balozi wa Kigoda cha Karume kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Ridhaa hiyo ameitoa huko ofisini kwake Mazizini mjini Unguja mbele ya Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) uliofika kuelezea hatua mbali mbali zilizofikia za kuelekea uzinduzi wa Kigoda hiki.
Dk. Karume aliipongeza Kamati ya Kigoda kwa kuibua wazo hili wakati muafaka ambapo Chuo kinatimiza miaka 23 tangu kilipoanzishwa.
‘’Muda mzuri sana, SUZA kwa sasa imekua kwa kuanza jambo hili’’, alisisitiza.
Alisema kuna taasisi kama hii imeundwa na umuhimu wake unaonekana inavyoeneza falsafa za Mwalimu Nyerere na kwamba inatumika vizuri.
‘’Tumeona umuhimu wa taasisi ile na kwetu yapo mengi sana ya historia ya Mzee Karume, unapoizungumza historia ya Zanzibar lazima Mzee Karume atakuwepo’’, alisisitiza.
Aliongeza kuwa yeye ndiye Rais wa Kwanza wa Zanzibar atakuwa na mchango mkubwa wa kuimarisha taasisi hii mbali na wanafunzi na wananchi kwa jumla.
‘’Wenye rika yangu ambao Mapinduzi na Muungano umetukuta tumebaki asilimia sita (6) tu (wamefariki), hapo utaona mahitaji ya historia yalivyo makubwa kwa vizazi vilivyopo na vijavyo ’’, alisema.
Aidha, Dk. Karume alisema yuko tayari yeye na familia yake kuunga mkono jambo hili ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
Mapema, Makamo Mkuu wa SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji alisema uzinduzi wa Kigoda cha Karume unatarajiwa kufanyika mapema mwezi wa Juni mwaka huu ambapo wasomi na viongozi mbali mbali wataalikwa.
Aliongeza kuwa lengo la kumuenzi Sheikh Abeid Amani Karume ni kuhifadhi, kuenzi na kuendeleza mawazo na fikra zake katika kuleta ukombozi na maendeleo ya Afrika.
‘’Taasisi hii itashughulika na masuala ya tafiti, makongamano kama hatua ya kumuenzi kwa ukombozi wa Tanzania na Afrika’’, alifahamisha.