Zanzibar yajivunia kuongezeka idadi ya wahitimu SUZA
Na Mwandishi Wetu, SUZA
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesifu jitihada za SUZA zinazochangia kuongezeka idadi ya wahitimu mwaka hadi mwaka katika Chuo hicho.
Akitoa hotuba yake mbele ya wahitimu, viongozi na wageni kwenye mahafali ya 19 katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Mwinyi alisema anaamini kuwa wahitimu hao wameandaliwa vyema ili kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira.
Akifafanua ongezeko hilo, Dkt. Mwinyi alisema katika mahafali haya wahitimu 2,012 wanapewa Shahada mbalimbali ikiwa ni sawa na asilimia tisa (9) ilinganishwa na idadi ya wahitimu 1,913 wa mwaka uliopita. Aidha, alipongeza jitihada za wanawake kuichangamkia sekta ya elimu ya juu ambapo kati ya wahitimu waliotunukiwa Shahada wanawake ni 1,229.
‘Napenda niupongeze uongozi wa Chuo, wahadhiri, wafanyakazi na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mafanikio ambayo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kinaendelea kuyapata katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu’, alisema.
Katika mahafali hayo, wahitimu 43 walitunukiwa Shahada za Uzamili, wahitimu 692 walitunukiwa Shahada za kwanza, wahitimu 999 walitunukiwa Stashahada na wahitimu 367 walitunukiwa astashahada.
Aidha, Dkt. Mwinyi ambaye pia ni Rais Wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameelezea kuridhishwa kwake na kuwepo programu mpya ya Ujasiriamali na Ubunifu (Bachelor of Enterprenuership and Innovation) ambapo wahitimu 18 amewatunuku Shahada zao wakiwemo wanawake 16 sawa na asilimia 89.
‘Nimepata faraja kuona kuwa Chuo kimeandaa maonesho ya ubunifu na jambo la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa wanapatikana watakaoweza kutumia elimu yao kubuni na kuvumbua kutakakosaidia kutatua changamoto za jamii, alisema Dkt. Mwinyi.
Katika mahafali hayo, Dkt. Mwinyi pia amemtunuku Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Usimamizi wa Utalii na Masoko ( Doctor of Philosophy in Tourism Management and Marketing -Honoris causa) kutokana na na mchango mkubwa alioutoa katika sekta ya utalii na maendeleo ya taifa.
Katika hatua nyengine, Dk Mwinyi aliwatunuku tunzo maalum za heshima viongozi wengine waliopanda mbegu za uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha SUZA ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango hao. Viongozi hao ni Rais Mstaafu wa Awamu ya tano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Salmin Amour Juma ambaye ndio kinara aliyetoa wazo hilo.
Wengine ni Mawaziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali katika vipindi tafauti Mhe. Haroun Ali Suleiman na Balozi Omar Ramadhan Mapuri. Aidha, aliyekuwa Katibu Mkuuwa Wizara hiyo kwa muda mrefu naye pia ana mchango mkubwa wa uratibu hadi wazo hilo likaanza kutekelezeka.
Mapema, akimkaribisha Mkuu wa chuo cha Taifa cha SUZA, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Leila Hassan ameelezea mafanikio yanayopatikana katika Chuo hicho kama vile kuwapatia mafunzo wahadhiri katika ngazi mbalimbali za mafunzo na Serikali kuwalipia ada za masomo wafanyakazi zaidi 100 wa Chuo hicho.
Aliongeza kuwa wahadhiri hao wapo masomoni kwenye ngazi mbali mbali kama vile Shahada ya uzamivu ( PhD) 47, Shahada ya Uzamili 37, Shahada ya kwanza 15 na Astashahada mwanafunzi mmoja.
Alifafanua kuwa kupitia Chuo cha SUZA imeanzisha maabara ya ubunifu WASTEX Lab Tunguu pamoja na kununu vifaa vya maabara vikiwemo kompyuta na vyengine vya Tehama.
Mapema, Makamo Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Moh’d Makame Haji aliipongeza jumuia ya Chuo ikijumuisha wanataaluma na wendeshaji kwa kazi nzuri wanayofanya ya kutoa wataalamu wa fani mbali mbali wanaotarajiwa kuwa mhimili mkubwa katika kuchangia ustawi wan chi.