Ziara za kimasomo  SUZA, Ostfold Norway zaimarika

Na Nasima Haji, SUZA

Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kimewateua wanafunzi  wanne  wanaosomea Stashahada ya Elimu ya Awali na walimu wawili kufanya ziara za kimasomo nchini Norway. Aidha, wanafunzi wengine watano na walimu wawili watatoka Norway kuja Zanzibar kwa lengo  la kubadilishana utaalamu.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya SUZA kupitia skuli ya  Elimu  na  Ostfold University College kutiliana saini ushirikiano  tangu mwaka 2019, makubaliano yanayojulikana kama  NoZa Intecultural Mobility.

Wakiwa Norway wanafunzi hao watapata fursa ya kutembelea sehemu mbali mbali  pamoja na kuhudhuria masomo darasani.

Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wanafunzi hao,  Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa Zanzibar (SUZA), Profesa Moh’d Makame Haji,  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaimarisha  elimu   kwa kuweka mazingira ya kuwawezesha vijana kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini.

‘Programu zinapata nguvu kubwa na ushawishi,  tuna uhitaji mkubwa na kwa vile elimu haimuachi mtu nyuma, ndio maana tunashajiisha kupatikana fursa hizi’, alisema.

Kutokana na umuhimu  wa masomo hayo na mahitaji ya  nchi  kwenye taaluma hiyo, Profesa Moh’d  aliwashauri wanafunzi kuzitumia fursa hizo ili kufikia malengo  yaliyowekwa.

‘Masomo  hayo ni adimu lakini ni muhimu katika sekta ya elimu kwani hatuna wataalamu  wa kutosha ambapo awali  hatukuweka mazingira  ya kupatikana wataalamu kwenye fani hiyo’, alisema Profesa.

Aliongeza  kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaimarisha  elimu   kwa kuweka mazingira ya kuwawezesha vijana kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini, hivyo ni vyema fursa hiyo wakaitumia inavyostahiki.

SUZA kina mipango mingi moja wapo ni kufanya makubaliano ya Umoja  baina ya Zanzibar na Norway ambako wakienda watakutana na wanafunzi kutoka mataifa mengine na wanapaswa wajifunze mazingira na utamaduni wenye maadili mema.

Aidha, aliwaonya wanafunzi hao kuwa SUZA haiko tayari kuharibu  uhusiano uliopo  na kwamba mtu asione ameenda Ulaya kuna maisha kisha akatoroka akakivunjia heshima, Chuo hakiko tayari yatokee hayo.

Mapema, Mkuu wa Skuli ya Elimu  Dk. said khamis juma, alifafanua kuwa mnamo mwaka  2022 wanafunzi wanne wa  Diploma ya  Elimu Mjumuisho na Mahitaji Maalum, Diploma ya Elimu ya Awali, walishiriki katika ziara hiyo  na  mwaka 2023  wanafunzi  sita wa Shahada ya Uzamili ya Elimu katika Vijana, Jinsia na Maendeleo walitembelea Chuo cha Ostfold kwa muda wa wiki tatu.

Aidha, wazazi wa wanafunzi ambao walishiriki katika hafla fupi ya kuwaaga wanafunzi hao iliyofanyika kwenye ofisi za SUZA, huko Tunguu waliushukuru uongozi wa  Chuo kwa kuwa simamia vyema wanafunzi wao ambapo Mzee wa mwanafunzi Abdultif Mussa Salum aliwanasihi wanafunzi hao kufuata maelekezo waliyopewa.

Hafla hiyo fupi ya kuwaaga wanafunzi ilifanyika mwishoni mwa wiki katika ofisi za SUZA kwenye  makao makuu yake huko Tunguu mwishoni mwa wiki iliyopita na wanafunzi  tayari wameelekea Norway kwa ajili ya kubadilishana utaalamu.

mwisho