TEHAMA kuondoa changamoto ajira kwa vijana

Na Nasima Haji, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema ofisi anayoiongoza inatengeneza sera ya TEHAMA kutatua changamoto ya ajira kwa vijana nchini.

Akihutubia kwenye kongamamo la kujenga uelewa kuhusiana na mradi wa GeoICT4e uliofanyika New Library katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Mwasaga alisema teknolojia mpya itatengeneza fursa kwa vijana ambapo kwa Tanzania vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 34 wanafikia milioni 21.

‘’ Vijana wetu hawa tukiwajengea uwezo, watapata ujuzi wanaotaka, unaoweza kufungua fursa katika masoko makubwa kwenye nchi za jangwa la Sahara (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).

Sambamba na kuweka mazingira bora ya mfumo wa upatikanaji na utumiaji wa teknolojia, alisisitiza ushirikiano baina serikali kuweka miundo mbinu ya kuchakata takwimu, sekta binafsi na vyuo vikuu kutengeneza takwimu.

‘Ukuaji wa mchango wa teknolojia ya ICT ni asilimia 74 na tunataka iwe kivutio kwa vijana katika uwekezaji’, alihimiza.

Aidha, alielezea umuhimu wa uhusiano uliopo baina ya Tanzania na Finland taifa lenye idadi ya watu milioni tano lililoendelea katika sekta ya teknolojia ya kisasa linalodhamini mradi huu wa miaka mitano.

‘Ili kuyafikia haya lazima tujenge ushirikiano na mataifa hasa ya nje, na sisi (Tanzania) tunajenga miundo mbinu hasa ya kukusanya takwimu’, alisisitiza.

Aidha, alizungumzia ushirikiano uliopo baina ya Kenya na Afrika ya Kusini ambapo mwaka jana Tanzania pia iliwapeleka vijana 10 kujifunza masuala ya ICT nchini Algeria.

Mratibu wa mradi huo, Dkt. Aboubakar Diwani wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) alisema mradi GEoICT ulipangwa kutekelezwa kwa muda miaka minne hadi kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka huu lakini ulisuasua kutokana na mripuko wa maradhi ya COVID-19 na baadaye kuendelea.

Katika mradi huo, SUZA huwajengea uwezo wanafunzi 50 kila mwaka ambao hupata fursa ya kujiajiri katika kazi mbali mbali za ukusanyaji wa takwimu, kuandika pendekezo la utafiti kufanya kazi za ushauri kwenye kampuni na masuala ya utandawazi.

Mradi huu unaodhaminiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, unatekelezwa kwa pamoja na vyuo vya SUZA, Chuo Kilimo cha Sokoine, Ardhi University, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. Kwa upande wa Finland, vyuo vinavyoshirikiana na Tanzania ni Chuo Kikuu cha Turku, Chuo Kikuu cha Novia na TUAS.

Wakuu wa vyuo hivi akiwemo Makamo Mkuu wa SUZA pia walishiriki katika kongamano hilo pamoja na maonesho yaliyofanyika katika jengo la New Library.

Mradi huu huwakusanywa vijana wenye taaluma mbalimbali na kushughulikia matatizo yanazikabili jamii na kuzipatia ufumbuzi unawajengea uwezo wa kujiamini, kuajirika na kujiajiri.

Akizungumzia kuhusu vijana ambao hawako kwenye vyuo, Dkt. Aboubakar alisema wao hufaidika na mpango huu kwa kushirikishwa na vijana wanaotoka vyuo vikuu kuchanganua mambo na kuyatafutia ufumbuzi

Katika mkutano huo, vijana kutoka vyuo vikuu kikiwemo SUZA waliwasilisha kazi na kuonesha michango wao katika jamii na maendeleo yao binafsi kwa kazi walizokuwa wakizifanya kwenye jamii.

MWISHO