SUZA, ZU na Sumeit kushiriki shindano  la sampuli za wanyama

 Na Mwandishi Wetu, SUZA

Vyuo vikuu vitatu vya Zanzibar, Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA),  Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) na  Chuo kikuu cha Sumeit vinatarajiwa kushiriki shindano la ubunifu la kutengeneza sampuli ya wanyama mashuhuri wa Tanzania ambao wanajulikana zaidi kwa jina la  ‘The Big 5’.

Wanyama hao ni Simba, Chui,  Nyati, Kiboko, na Ndovu  watakaokuwa na urefu wa sentimita 15 ambao watatengenezwa kwa kutumia  takataka ngumu (recycling) ili

kuishawishi jamii kutambua umuhimu wa uhifadhi mazingira.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia matokeo ya utafiti ukiofanywa mwaka 2019 ambao uliwasilishwa na  Meneja wa Kampuni ya  Cocon  Collection  inayosimamia kisiwa cha Bawe, Mehdi Ahmed.

 Ahmed alisema kwa mujibu wa utafiti huo  kati ya wageni watano wanaoitembelea Zanzibar wanne kati yao  wanaapa kutoitembelea tena nchi hii kutokana na uchafu.

 ‘’Uchafu huo unatuathiri sana  Zanzibar na tunapaswa kubadilisha mtazamo wa watu kuhusiana kuweka usafi  wa mazingira’’, alisema.

 Aliongeza kuwa shindano lifanyika kwa kutumia taka taka kama vile, chupa, vizibo vya soda, unga wa mbao, makapi ya muwa, makaratasi na kadhalika.

 Alisema kuwa kila Chuo kinatakiwa kuwa na washindi watano ambao watazawadiwa  kwa kazi zao hizo akiwemo mshindi wa kwanza ambaye atapata fursa ya ya ufadhili wa kuvitembelea visiwa vya Maldives.

Alifahamisha kuwa   shindano    hilo limeanza  18/04/2024 na litadumu kwa muda wa siku 50 hadi tarehe 5 Juni mwaka huu ambapo mnamo Septemba 15 mwaka huu washindi hao watazawadiwa tunzo zao katika uzinduzi wa  hoteli  katika kisiwa cha Bawe.

Katika uzinduzi huo, ambao utawashirikisha mahakimu wa kimataifa wa shindano utahudhuriwa pia na viongozi wa ngazi za juu wa Zanzibar.

Mhadhiri mwandamizi wa SUZA, Dk. Aboubakar Diwani Bakar, alisema katika kumbi za SUZA kuwa Chuo kinaleta fursa huru ili kila mmoja aweze kushiriki na kuonesha kipaji chake.

 ‘’Najua mna vipaji, mnaweza mkaona hili ni jambo dogo lakini linaweza likaleta manufaa makubwa hasa kwa wale ambao wanalalamikia ajira’’, alisisitiza.

Katika hatua nyengine, Kampuni hiyo imetangaza nafasi nne za kazi kwa wazawa ambapo sifa kuu ni uwezo wa kuchapa kwa kutumia kompyuta na  kuzungumza lugha za kigeni  ikiwemo kiingereza.