SUZA wapewa jukumu kupitia sheria za bahari

 

Na Nasima Haji, SUZA

Mwenyekiti wa Kamati ya   Baraza la Wawakilishi,  Kepteni Abdallah Hussein Kombo,  ameuagiza uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kushirikiana na wadau kupitia sheria za matumizi bora ya bahari ili kufikia malengo na vigezo vya kimataifa.

Akizungumza katika kikao  cha mradi  wa  kuwajengea uwezo  vijana kujiajiri  na kuajirika  katika soko la uchumi wa buluu Zanzibar (Skills Development for Youth Employability in the Blue Economy– SEBEP),  kilichofanyika huko Maruhubi mwishoni mwa wiki.

Alisema sheria hizo hazikidhi haja kwa sababu   sera ya matumizi ya bahari tayari imebadilishwa na kwamba iko haja  ya sheria kuendana na matakwa ya matumizi ya bahari yanayotakiwa hivi sasa.

‘’ Jitihada mbali mbali zilifanyika  kubadilisha sheria lakini hazikufanikiwa, sasa hili ni suala la nyinyi SUZA kuwaita wadau kuijadili, kutoa maoni yao ili kutengeneza mchakato wa kuona wapi tunataka kwenda’’ , alisisitiza

Kuhusu matumizi ya bahari, alihimiza kuwepo  mtaala maalum wa kuielimisha jamii namna bora ya kuitumia kwa  ajili ya kuwawezesha watu wengi zaidi kufaidika na hazina hiyo.

Akizungumzia kuhusiana na uhifadhi wa mazingira alikumbusha kuwa kuna umuhimu wa kuweka   kikosi  cha kuangalia usafi wa mazingira  hasa ikizingatiwa kuwa zipo taasisi  nyingi zinazohusika kuangalia ustawi wa matumizi bora ya bahari na rasilimali zake.`

Mapema, Makamu Mkuu wa SUZA, Profesa Moh’d Makame Haji, wakati akimkaribisha mgeni rasmi wa warsha hiyo alisema SUZA kimepewa jukumu na  uongozi wa awamu ya  nane  unaoongozwa na Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuongeza nguvu katika ustawi wa uchumi wa buluu, kuvuna bidhaa za bahari ikiwa ni pamoja na  kuvuna mazao ya bahari na kudumisha uhusiano baina ya pande mbili.

’’ Mradi huu  wa    SEBEP  unatupa fursa na nguvu ya kuhakikisha kuwa tunaweza kuyafikia malengo yetu.

Miongoni mwa malengo hayo ni kuimarisha ubora na ufanisi wa upatikanaji wa taaluma, kuongeza kiwango cha ajira kwa vijana kwa kutumia rasilimali zake za Zanzibar za asili, kuimarisha taaluma ya ujasiriamali   

Akiwasilisha mada kuhusu kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika katika soko la Uchumi wa Buluu Zanzibar, Mratibu wa mradi huo kutoka SUZA, Dkt. Yahya Hamad Sheikh, alisema mradi huo utachangia kupunguza ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira Zanzibar.

Akitoa takwimu za mtiririko wa vijana wasiokuwa na ajira mwaka mwaka 2006   lilikuwa 379,038 hadi kufikia 568,094 mwaka 2021 ambao ni vijana wenye umri wa miaka 15 -35 imeongezeka kutoka asilimia 19.6 (2006) hadi asilimia 27.4 (2021).  Huku vijana wanawake  wasiokuwa na ajira inakadiriwa  kufikia asilimia 40.6 kwa mwaka (2021) kutoka asilimia 15.4 (2006).

‘’ Serikali inalenga kuwapatia vijana ujuzi unaokubalika  katika soko la ajira  linaloweza kuwapatia ajira wakiwa wameajiriwa au kujiajiri’’, alisema.

Naye Raya Juma Khalfan, mwakilishi kutoka  jumuia ya wanawake mabaharia alishauri kuwepo  Chuo kitakachowafundisha mabaharia wanawake kwani wamekuwa wakishindwa kujipatia elimu nje ya Zanzibar kutokana na gharama kubwa za masomo ya ubaharia na usafiri nje ya Zanzibar.

‘’Wanawake wengi wanavutiwa na kusoma  ubaharia lakini wanashindwa kutokana na  gharama za mafunzo, yakitolewa hapa Zanzibar yatasaidia’’, alisema.

Khamis Rashid ambaye ana uzoefu katika masuala ya ubaharia alisema kwa masikitiko kuwa asilimia 80 ya mabaharia wa Zanzibar ni kutoka Tanzania bara ambapo Zanzibar imeshawaandaa vijana wengi mabaharia ambao hawatumiki.

‘Cheti hakitoshi, uzoefu ni muhimu  na wenye uzoefu wapo tuwatafute, hatuwatumii na mwisho wake watatukimbia,’’ alisema  baharia mzoefu, Khamis Rashid.

Aidha, alipendekeza kuwa ni vyema taasisi inayosimamia ustawi wa masuala ya  baharini ikatafuta vifaa kwani wataalamu wapo wa kutosha ambao wamekuwa wakitumika endapo zinatokea kazi za dharura kwenye meli.

Mradi wa huu unaotarajiwa kugharimu  shilingi 125b utagharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa asilimia 90 na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia 10  umeanza utekelezaji wake mwezi Mei mwaka jana na kukamilika mwezi Septemba mwaka 2027.

mwisho