SUZA,  Qatarairways  wakubaliana kushirikiana

Na Nasima Haji, SUZA

CHUO Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na uongozi  wa Shirika la Ndege la Qatarairways wamekubaliana kushirikiana kwa  viongozi, walimu, wafanyakazi na wanafunzi kutumia huduma ya Shirika hilo kwa punguzo maalum.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Moh’d Makame Haji, amelishukuru Shirika hilo kwa kuitambua SUZA na kuwa tayari kuunda ushirikiano huo kwa kupata punguzo na nyongeza ya mizigo kwa jamii ya SUZA.

Alifahamisha kuwa SUZa ina programu mbalimbali za ushirikiano na vyuo na mashirika ya kimataifa   kitaaluma ambapo watendaji wake hulazimika kusafiri mara kwa mara kwa  ajili ya masomo,  mikutano na ubadilishanaji wataalamu katika fani mbalimbali.

‘’Tunashirikiana nao, tuna mpango wa kubadilishana wataalamu na hivi karibuni wanafunzi wetu 10 waliondoka nchini’’, alisema.

 Aliongeza  kuwa kuwepo mpango maalum wa kupunguza gharama utaisaidia serikali   hasa kwa vile SUZA ina wataalamu wengi ambao Chuo kinaidhinisha maombi yao ya safari.

‘’Wazo lenu ni zuri hatuna shida nalo sasa mazingira ya tunaanza vipi  ndio ya kuangaliwa’’, alisema Profesa.

Meneja wa  Shirika hilo, Julieth Makonyi alisema wanafunzi wakiungwa katika Club na kupatiwa namba ya utambulisho wataweza kupatiwa punguzo la asilimia 10  kwenye tiketi  sambamba na kupatiwa nyongeza ya kilo kwa mizigo yao.

‘’ Huduma hizi pia zitapatikana kwa viongozi wakuu wa SUZA na walimu wao’, alisisitiza, Meneja wa  Shirika hilo, Julieth Makonyi.

Alifafanua kuwa mpango huu hautaathiri mahusiano ya Chuo na wakala wengine wa tiketi za ndege kwani mfumo huo utaunganishwa kwa wakala wanaotumiwa na SUZA.

MWISHO