SUZA na Ubalozi wa Marekani Tanzania kuimarisha mashirikiano
Kazi kubwa kwa sasa Uongozi wa Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar ni kuongeza wigo wa kukitangaza Chuo kimataifa ikiwa pia utekelezaji wa dira na dhamira ya kuwa Chuo kinachotambulika ulimwenguni.
Hayo yamesemwa Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Moh’d Makame Haji alipokutana na Bw. Jackson Oganda Mshauri wa Masuala ya Elimu kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.
Bw. Oganda alikuja kuonana na Makamu Mkuu akiwa na lengo la kuimarisha mahusiano na kuainisha fursa mbalimbali ambazo SUZA itanufaika kupitia Ubalozi zikiwemo nafasi za ufadhili wa masomo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu, kubadilishana wanataaluma na wanafunzi wa Marekani kuja SUZA na wa SUZA kwenda Marekani, kushirikiana kwenye tafiti mbalimbali.
Kwa upande wake Prof. Moh’d amesema kuwa ujio wake ni mzuri na unafungua mlango mwingine wa mashirikiano ambapo mwaka jana Ubalozi ulifanya ukarabati wa jengo la Chuo lililopo Kampasi ya Vuga na kurejesha huduma za maktaba (American corner) zilizokuwa zimesitishwa kwa muda mrefu.