SUZA KINASHIRIKI MAONESHO YA 47 YA SABASABA

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kinashiriki maonesho ya 47 ya kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika katuka viwanja vya Sabasaba vilivyopo Barabara ya Kilwa Dar es Salaam. Maonesho haya yameandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania yanajumuisha washiriki mbali kutoka Wizara, Taasisi, Mashirika ya Umma na Binafsi, Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya Tanzania zaidi ya Makampuni 114 yanashiriki.

Katika kutekeleza jukumu lake la kuchangia maendeleo ya nchi na kutatua changamoto mbali mbali kwenye jamii, Chuo kupitia Idara ya Sayansi ya Kompyuta na TEHAMA inaonesha sampuli mbili zilizotengenezwa kwa kutumia Teknolojia ya IoT (Internet of Thing). Sampuli ya kwanza inakwenda kutatua changamoto ya usimamizi wa ufugaji wa kuku wa kisasa. Sampuli hii inahusisha matumizi ya Teknolojia ya IoT pamoja na Akili bandia (AI) kurahisisha na kuongeza ufanisi katika ufugaji wa kuku. Vifaa vilivyofungwa kwenye banda la kuku vina uwezo wa kuangalia, kupima, na kusawazisha kiwango cha joto, maji, chakula pamoja na kugundua iwapo kuna mtu amefungua mlango wa banda la kuku bila ya ruhusa ya mmiliki ambapo mfumo utatoa taarifa za moja kwa moja kupitia simu ya mkononi ya mmiliki wa kuku. Aidha, kupitia mfumo huu, mfugaji anauwezo wa kufatilia ukuaji wa kuku wake wakati wote na popote alipo.

Sampuli ya pili nayo imehusisha Teknolojia ya IoT pamoja na AI inakwenda kutatua changamoto ya kuchelewa au kukosa huduma ya afya kwa wagonjwa wenye kiwango kikubwa cha homa kutokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa kwenye vituo vya afya na hospitali. Mfumo huu unahusisha vifaa vinavyoweza kupima hali ya kiafya ya mgonjwa kupitia viashiria vya afya kama vile joto la mwili, mapigo ya moyo, na kiwango cha oksijeni kwenye damu. Vifaa vya upimaji vinachukua taarifa za mgonjwa. Mgonjwa anatakiwa kuweka vidole vyake kwenye vifaa vya upimaji ambapo majibu ya vipimo vyake yanatumiwa na Akili bandia kuwekwa katika kundi maalum la kupata huduma kutoka kwa daktari. Wakati huo huo, vipimo vya mgonjwa vinatumwa kwa daktari moja kwa moja na kama hali yake ni mbaya kulinganisha na wagonjwa wengine daktari anaweza kumuita mgonjwa huyo kwanza kabla ya wengine.

Pamoja na kuonesha sampuli za hapo juu chuo pia kinatoa huduma ya udahili kwa program zake mbalimbali kwenye kada tofauti ikiwemo Afya, Utalii, Sayansi Asili Sayansi Jamii, Kilimo, TEHAMA, Uandishi wa Habari, Sayansi ya Kompyuta, Biashara, Benki, Ualimu wa Syansi na Sanaa, Sanaa, Lugha mbalimbali kama vile Kichina, Kikorea, Kifaransa, Kiingereza, Kiarabu n.k.

Maonesho haya yameanza tarehe 28 Juni, 2023 na yanatarajiwa kumalizika 13 Julai, 2023.