SUZA, Fulbright kuanzisha ushirikiano wa kitaaluma

Na Nasima Haji, SUZA

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kimekubaliana na Taasisi Fulbright ya Marekani  kuanzisha ushirikiano wa kuandika kazi za kitaalamu na kitaaluma.

Ushirikiano huu utawaleta wataalamu wa fani hiyo  kutoka  katika taasisihiyo kwa kushirikiana na SUZA katika Kurugenzi ya  Shahada ya Juu, Tafiti na Ushauri Elekezi.

Katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa Makamo Mkuu wa Chuo  cha SUZA, Profesa Mohammed Makame Haji, alisema SUZA imeona fursa na inaweza kuomba  wanafunzi wa SUZA wataongezewa ujuzi wa kuandika ripoti, wazo wa utafiti (concept note), pendekezo la utafiti (proposal), tasnifu (dissertation) na maandiko mengine ya kuchapishwa kwenye jarida.

‘’ Tumekubali ushirikiano na tunaunga mkono wazo hili, tumeona  faida zake na SUZA iko tayari’’, alisema Profesa.

Naye mtaalamu kwenye fani ya uandishi Juli Nelson amesema kuwa vyuo vingi vimekuwa vikitekeleza mpango wa kuwajengea uwezo wanafunzi wao kuelekea kwenye uandishi bora wa maandiko mbali mbali ikiwa ni pamoja na miradi, kazi za skuli na ripoti.

Wakati  huo huo, Professa Moh’d ametiliana saini na hati ya maelewano ya ushirikiano katika maeneo ya utafiti, afya, na maendeleo ya elimu  baina ya SUZA na Shirika la Pharm Access international  linaloongozwa na  Mkurugenzi Mkaazi  Tanzania,  Dkt. Heri Marwa.

Ushirikiano  huo utahusu kufanya tafiti  kuhusiana na  afya mama na mtoto, ubora wa utoaji huduma  za afya na masuala ya afya kwa jamii kwa jumla.

Katika hatua nyengine, matokeo ya tafiti yatasambazwa kwa wadau mbali mbali ndani na nje ya nchi.