HOTUBA YA MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR AMBAYE PIA NI RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI: MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN KATIKA MAHAFALI YA KUMI NA NNE: TAREHE 23 APRILI, 2019

Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar; Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Baraza la Wawakilishi; Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali; Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, Waheshimiwa Mawaziri Mliohudhuria,

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; Mheshimiwa Said Bakari Jecha,

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; Profesa Idris Ahmada Rai,

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja; Mheshimiwa Hassan Khatib Hassan,

Ndugu Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mheshimiwa Ramadhani Abdallah Ali,

Ndugu Wahadhiri na Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Ndugu Wanafunzi na Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana

Assalamu Aleikum

Awali ya yote, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu; Subhanahu Wataala aliyeumba Mbingu na Ardhi na vyote viliyomo ndani yake, kwa kuturuzuku neema ya uhai na afya njema tukaweza kujumuika katika sherehe za Mahafali ya Kumi na Nne, ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, leo tarehe 23 Aprili, 2019. Tunamuomba Mola wetu aujaalie baraka mkusanyiko wetu huu na atuwezeshe kuifanya shughuli hii kwa furaha, salama na amani tangu mwanzo hadi tutakapoikamilisha.

Pili, nikiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar pamoja na wanajumuiya wote wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar nakukaribisheni wageni na waalikwa nyote katika shughuli hii ambayo kama kawaida yake imefana sana. Nakupongezeni nyote wageni mlioalikwa kwa kuhudhuria kwa wingi katika shughuli yetu, jambo ambalo linatupa faraja kuwa nyote mnauona umuhimu wa sherehe hizi kwa mustakabal wa wahitimu wetu, chuo na jamii yote kwa jumla. Kwa niaba ya chuo, nasema; Ahsanteni sana!

Tatu, natoa shukurani maalumu kwa vijana wetu wahitimu kwa kuonesha moyo wa uvumilivu na subira mliyoionesha kutokana na kuchelewa kufanyika kwa Mahafali haya ya kumi na nne. Kwa hakika, mmeonesha ukomavu mkubwa na uzalendo katika kipindi chote mlichosubiri hadi leo tumeweza kufanya mahafali haya. Hongereni sana kwa kuuzingatia usemi wa wazee kwamba; “Kawia ufike kwaniharaka haraka haina baraka”. Tulilazimika kuchelewa kidogo, ili tuweze kufanya marekebisho ya ukumbi huu na kupata mahali pazuri panapofaa kwa kufanyia mahafali haya. Nakupongezeni sana kwa ustahamilivu mliouonesha.

Nimefurahishwa na hali ya ukumbi ilivyo kwa sasa baada ya utekelezaji wa agizo langu la kuuendeleza ukumbi huu wa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuufanyia marekebisho mbali mbali kutokana na hitilafu zilizobainika baada ya kuanza kutumika katika Mahafali yaliyopita. Leo, sote tunashuhudia namna tulivyoweza kupunguza kiwango cha joto katika ukumbi huu; tofauti na hali ilivyokuwa mwaka jana. Hongereni sana. Ni mategemeo yangu kuwa ukumbi huu mtautunza, ili uweze kutumika vyema kwa mahafali yajayo na shughuli mbali mbali za maendeleo ya chuo, na shughuli nyengine za nchi yetu za kitaifa na kimataifa.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Tumekutana hapa katika mkusanyiko huu wa Mahafali tunaoufanya kila mwaka, ili kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa majukumu ya Chuo chetu ya kutoa elimu ya fani na ngazi mbali mbali hapa Zanzibar. Shughuli kubwa tunayoifanya katika hadhara ya leo ni kuwatunuku vyeti wahitimu wa fani mbali mbali za masomo yanayofundishwa katika kampasi zote za Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kuanzia ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada ya kwanza, Shahada ya Uzamili hadi Shahada ya Uzamivu ya Kiswahili

Kwa hakika, tunastahiki kujipongeza kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi ya nguvu kazi yenye taaluma, ambayo ni chachu ya kuongeza kasi ya maendeleo nchini. Nawapongeza viongozi wenzangu wa Chuo, wahadhiri na wafanyakazi wote wa Chuo hiki kwa kufanya kazi nzuri inayotuwezesha kupiga hatua zaidi za mafanikio hapa Chuoni mwaka hadi mwaka. Kadhalika, natoa pongezi maalumu kwa wahitimu wote ambao wametunukiwa Shahada zao na wengine pamoja na zawadi, katika Mahafali haya kutokana na bidii na nidhamu zao, ambavyo ndio siri ya mafanikio katika kutafuta elimu. Vile vile, nawapongeza wazazi na walezi wa wahitimu wote waliotunukiwa shahada zao leo kwa mafanikio ya vijana wetu, ambayo kwa hakika yamechangiwa na jitihada za wazazi hao katika kuwahudumia na kuwahimiza kuzidisha bidii katika masomo yao. Hongereni sana.

Tumeelezwa kwamba katika Mahafali ya mwaka huu zipo jumla ya fani za masomo 56 zenye wahitimu 1940. Asilimia 58 ya wahitimu wote ni wanawake na asilimia 42 ndio wanaume. Kwa mara nyingine mwanamke ametokea kuwa mwanafunzi bora; kwa hakika, mmethibitisha kuwa wanawake mna uwezo mkubwa. Hongereni sana.Matokeo haya ni kielelezo cha jitihada za wanafunzi wa kike katika masomo yao na hasa katika kuhakikisha kuwa wanawake nao wanapata fursa na kufaulu vyema kwenye taasisi za elimu ya juu katika fani mbali mbali za masomo.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Miongoni kwa faida kubwa za kuwepo kwa vyuo vikuu ni kuhakikisha kuwa vinazingatia na kuweka mbele mahitaji ya msingi ya jamii. Kwa kutekeleza shughuli za vyuo vikuu kitaaluma, Taasisi hizi za elimu ya juu hulazimika kuwa na uwezo wa kufanya mabadiliko kulingana na mahitaji ya jamii. Vile vile, ni dhahiri kuwa katika enzi hizi, Chuo Kikuu ni lazima kiweze kutoa taaluma yenye umahiri yenye lengo la kuleta ustawi bora wa maisha ya jamii na kuchochea maendeleo yake. Kwa mnasaba wa maelezo haya, ni jambo la kutia moyo kuona Chuo chetu kinaendelea kuvizingatia vigezo hivyo muhimu. Tumekuwa tukishuhudia kila mwaka kunakuwa na ongezeko la fani mpya za wahitimu. Nimefurahi kusikia kwamba kwa mara hii lipo ongezeko la wahitimu wa fani mbili mpya. Fani hizo ni Shahada ya Utabibu (Doctor of Medicine) ambao idadi yao ni 25 na wahitimu 53 wa Cheti cha Uanagenzi (Apprenticeship) kwenye fani ya utalii. Hata hivyo, kuna haja ya kufikiria upya jina la fani hii ya Uanagenzi. Haipendezi wahitimu hawa kuja kusema wanacheti cha uanagezi baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu. (Ni vyema tukaitafakari upyatafsiri ya neno hili la “Apprenticeship”, sio lazima tukawa kila kitu tunakipa jina kwakutafsiri majina kutoka lugha za kigeni).

Natoa shukurani maalum kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuiendesha Programu ya Uanagenzi katika fani ya utalii kwa ufanisi mkubwa. Naamini kwamba wahitimu wote wametayarishwa vizuri na wako tayari kushirikiana na Serikali katika kuiendeleza sekta ya utalii ambayo hivi sasa ndio muhimili mkuu wa uchumi wetu.

Ni dhahiri kuwa kuhitimu kwa wanafunzi wa Shahada ya Utabibu ni taarifa njema na yenye kutia moyo. Wako waliodhani kwamba hatutoweza kuwafundisha madaktari hapa Zanzibar katika chuo hiki kwa sababu mbalimbali. Nataka nikiri kwamba haikuwa rahisi kuyaanzisha masomo hayo kwenye chuo chetu hiki. Hata hivyo, tulidhamiria, tulivinjari na tumeweza. Leo vijana wetu hawa tayari wamehitimu kama vile tulivyopanga Serikalini. Mafaniko haya yatatuwezesha kupata ufumbuzi changamoto ya uhaba wa madaktari nchini kwetu. Kwa hakika, tutaendelea kupiga hatua ya mafanikio katika sekta ya afya kwa kuongeza idadi ya madaktari kila mwaka. Hivi sasa daktari mmoja anahudumia watu 6,435 (1:6435) ikilinganishwa na watu 23,000 (1:23,000) kwa daktari mmoja katika mwaka 1997. Lengo lilowekwa na Chama cha Afro Shirazi hapo 1965, katika mpango wa mwanzo wa huduma za afya lilikuwa ni daktari mmoja ahudumie watu Elfu Sita (1:6000). Baada ya muda mrefu kupita, sasa tumeanza kufanikiwa.

Ni mategemeo yangu kuwa uongozi wa Wizara ya Afya utaendelea na utaratibu wa kuwaajiri madaktari wetu kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi Serikalini kwa lengo la kuziimarisha huduma za afya ikiwemo kupunguza tatizo la uhaba wa madaktari katika hospitali zetu. Ni wazi kuwa kupatikana kwa wataalamu hawa, kutaongeza uwezo wa hospitali zetu katika kutoa huduma zilizo bora zaidi na kuitekeleza

mipango mbali mbali tuliyodhamiria kuyatekeleza, likiwemo suala muhimu sana la kupunguza idadi ya vifo ya watoto na wanawake vitokanavyo na uzazi. Kwa namna ya pekee naipongeza Wizara ya Afya kwa kulitekeleza agizo langu nililowataka wahakikishe kuwa Hospitali ya Mnazi Mmoja inatumika kwa kufanya mafunzo yamazoezi ya madaktari wanaohitimu yaani “internship”; kama ilivyoamuliwa tangumwaka 1977.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Ni jambo la faraja na kutia moyo kuona kuwa jitihada zetu za kuandaa wataalamu wa Shahada za Juu za Lugha ya Kiswahili zinazidi kupata mafanikio. Katika mahafali ya mwaka jana tulipata wahitimu watano wa Shahada ya Uzamivu ya Kiswahili. Kwa mara hii nimeelezwa kuwa tunao wahitimu wengine wa Shahada ya Uzamivu watano (5) na wahitimu wanane (8) wa Shahada ya Uzamili ya Kiswahili. Kwa takwimu hizi, ni dhahiri kuwa nchi yetu inazidi kupata mafanikio katika jitihada zetu za kuongeza wataalamu wa Isimu na Fasihi ya Lugha ya Kiswahili kila mwaka. Hatua hii ni muhimu sana katika kufikia malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha kuwa Zanzibar kupitia SUZA, inakuwa ndipo wanapoandaliwa wataalamu bora na mahiri wa Lugha ya Kiswahili. Hatua hio itaiendeleza Zanzibar kuwa chemu chemu ya Kiswahili sanifu na fasaha.

Kutokana na idadi hii kubwa ya Wataalamu wa Lugha ya Kiswahili wa Uzamivu na Uzamili, hivi sasa Zanzibar tuna rasilimali kubwa ya wataalamu wetu wa Lugha ya Kiswahili. Nasaha zangu ni kuwa tuitumie vyema rasilimali hii kwa kuwashirikisha Wazanzibari wanaoishi nchi za nje na kuweka mikakati maalum ya kuikuza Lugha ya Kiswahili na kubainisha uwezo wetu wa kuwafundisha watu wa mataifa mengine wanaohitaji kufundishwa Kiswahili kilicho fasaha na sahihi. Nafahamu kwamba kuna mahitaji makubwa ya lugha ya Kiswahili katika kuimarisha mawasiliano ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo Afrika ya Kusini ambayo tayari imeshatangaza kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili katika skuli za nchi hio. Kutokana na hali hio, ni vyema sasa tukajipanga vizuri katika kuzichangamkia fursa hizo, ili ziweze kutusaidia katika kujijenga kiuchumi. Hata hivyo, nawahimiza wahitimu na wataalamu wetu wa Kiswahili wafanye jitihada, ili wajiandae kwa kuzitafuta fursa zilizopo za mahitaji ya wataalamu wa Kiswahili badala ya kukaa na kusubiri Serikali kuwatafutia fursa hizo.

Kadhalika, itakumbukwa kuwa nilisema katika kongamano la kwanza la Kiswahili la Kimataifa, lililoandaliwa na BAKIZA mwaka juzi, kwamba Taasisi hio ishirikiane na SUZA katika kuhakikisha inaandaliwa mikakati ya kuongeza idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaokuja kujifunza lugha ya Kiswahili hapa Zanzibar; kwani inaonekana kuwa kwa sasa idadi ya wanafunzi tunaowapata hailingani na hadhi yetu. Sijaelezwa hadi sasa agizo hilo limefikia hatua gani katika utekelezaji wake, ila kutokana na umuhimu wake katika dhamira yetu ya kuwa “wataalamu tuliobobea katika Kiswahili”hapa Zanzibar, napenda nilisisitize tena jambo hilo katika hadhara hii.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Nimefurahi kusikia kuwa kwa mwaka huu wa masomo, Chuo kitazindua udahili wa program mpya mbili katika ngazi ya Shahada ambazo ni Shahada ya Sayansi ya Uuguzi (DSc. Nursing) na Shahada ya Sayansi za Kilimo. Nakupongezeni sana kwa uamuzi wenu huo. Mpango wa kuanzisha Shahada ya Sayansi ya Uuguzi unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuimarisha afya ya mama na mtoto. Vile vile, fani ya Sayansi ya Kilimo ni muhimu katika juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuimarisha kilimo kwa kutumia njia za kisasa zenye kutilia mkazo matokeo ya tafiti mbali mbali.

Serikali iliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, ikiunganishwe Chuo cha Kilimo cha Kizimbani na SUZA. Nimefurahi kuona kwamba utekelezaji wa mpango wa kukiunganisha Chuo cha Kilimo Kizimbani na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) uko katika hatua za mwisho kukamilika. Hapana shaka uongozi wa chuo ukatumia uzoefu uliokwishapatikana katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati tulipoziunganisha Taasisi nyengine kuwa sehemu ya SUZA, ili isionekane kuwa jambo hili linasababisha usumbufu. Mpango huu bila ya shaka utazidi kuziongezea hadhi ya kitaaluma Taasisi zote zilizopo SUZA.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Nimefurahi kusikia taarifa za Makamu Mkuu wa Chuo, kuwa upo mpango maalumu wa kuyafanyia matengenezo makubwa majengo ya chuo kwa asilimia 75 na kujenga majengo mapya 12. Serikali imejiandaa kuutekeleza mpango huu, ili ufanikiwe; mpango mkakati huo wenye lengo la kuimarisha miundombinu, katika Kampasi zetu, ikiwemo kushughulikia majengo na vifaa vya kufundishia pamoja na kukuza utaalamu wa wafanyakazi na wakufunzi. Miundombinu ya chuo yakiwemo majengo lazima yatunzwe kwa kuweka utaratibu wa kuyafanyia matengenezo ya mara kwa mara na ndipo yatakapoweza kudumu. Tuzingatie usemi mashuhuri wa Wazeeusemao; “Kitunze, kidumu”. Kwa kukosa utunzaji mzuri wa baadhi ya majengo yetuya Chuo hasa yale yaliyorithiwa kutoka Taasisi za hapo kabla, majengo yetu hayo hivi sasa yanaonekana kuchakaa sana. Sina haja ya kusema yako wapi, ila najua na nyinyi mnayaona. Tusisahau kuwa majengo hayo zikiwemo nyumba za wafanyakazi tunazo chache na vile vile Chuo kina uchache wa nafasi za kufanyia kazi, tunahitaji dakhalia kwa wanachuo pamoja na vifaa vya kisasa vya kufundishia hasa kwa masomo ya Sayansi.

Ilivyokuwa, suala hili ni letu sote ni wajibu wa kila mmoja wetu achukue hatua zinazofaa. Serikali itashirikiana na uongozi wa Chuo katika kutekeleza wajibu wake wa kutafuta uwezo wa kuyafanyia matengenezo baadhi ya majengo na kuongeza majengo na vifaa. Vile vile tutatafuta nyenzo zaidi pamoja na nafasi za masomo kwa ajili ya walimu na wataalamu wengine, ili kukiwezesha chuo chetu kutoa elimu bora zaidi na inayokidhi mahitaji ya nchi yetu.

Sote tunafahamu umuhimu na majukumu ya wahadhiri katika kuwaendeleza wanafunzi wa Chuo Kikuu. Hata hivyo, nnazo taarifa kwamba kuna baadhi ya wahadhiri wachache kwenye Chuo chetu cha SUZA, ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo. Wapo ambao hawaonekani kwenye vipindi vyao wakati wa masomo, wapo wanaoingia darasani bila ya matayarisho, wengine wanawaambia wanafunzi wasome kwa kutumia mitandao bila ya kuwapa miongozo muhimu na kadhalika. Uongozi wa chuo, una kazi ya kuwaweka sawa wahadhiri hawa na wafanyakazi wote wanaojaribu kufanya kazi zao kinyume na utaratibu. Wahadhiri, walimu na

wafanyakazi wa namna hawatimizi wajibu wao vizuri na hawachangii maendeleo ya chuo. Wafanyakazi wa namna hii hawana uzalendo. Si wazalendo na hawastahiki wajigambe kuwa ni wahadhiri wa SUZA. SUZA ni chuo cha watu wenye kuyapenda maendeleo ya viongozi wa baadae.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Ili tuendelee kupata mafanikio zaidi, vile vile, nakunasihini tudumishe umoja na mshikamano uliopo baina ya wahadhiri, wafanyakazi wanafunzi na washirika wote wa chuo hiki. Tuendelee kujiepusha na mambo yanayoweza kuleta mifarakano. Kwa hakika umoja wetu, ndio ngao yetu. Ni wazi kuwa mafanikio ya chuo hiki yataletwa kwa maelewano na kwa kila mtu kutekeleza ipasavyo wajibu wake. Sheria na taratibu zilizowekwa katika kuendesha chuo hiki, ndizo zikuongozeni katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku ya chuo. Mwenendo huo peke yake ndio utakaokifanya Chuo chetu kiendelee kuwa miongoni mwa vyuo bora na chenye kutoa wahitimu wenye uwezo wa hali ya juu wa kitaaluma.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Kwa nyakati mbali mbali, nimekuwa nikizungumza na washirika wetu wa maendeleo wakiwemo viongozi wa nchi, mabalozi na Taasisi mbali mbali juu ya namna wanavyoweza kushirikiana nasi katika kukiendeleza Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Nafanya hivyo, kwa kuzingatia kuwa mimi ndiye Mkuu wa chuo hiki na Rais wa Zanzibar na maendeleo ya SUZA yana nafasi maalum kwangu katika kipindi chote cha uongozi wangu. Chuo chetu kinashirikiana na vyuo mbali mbali duniani na tumetiliana saini za Maelewano (MoU) katika kushirikiana huko. Uongozi wa Chuo chetu ni vyema ukaongeza kasi katika kufuatilia utekelezaji wa Nyaraka za Maelewano (MoU) tunazoingia na Taasisi nyengine. Hatua hio ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa shughuli za Chuo hiki na kuendeleza mahusiano mema kati ya Chuo chetu na Taasisi hizo.

Nataka nirudie tena kwamba Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake, ili tuweze kuyafanikisha malengo yetu kwa kutumia fedha zetu za bajeti na mipango mengine ambayo imeungwa mkono na nchi marafiki na washirika wetu wa maendeleo. Vile vile, mafanikio ya Chuo chetu, yanatokana na michango tunayoipata kutoka kwa Washirika wetu wa Maendeleo. Natumia fursa hii kutoa shukurani kwa Washirika wetu wote wa Maendeleo kwa misaada yao mbali mbali wanayoitoa katika kuchangia maendeleo ya SUZA.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Kama ilivyo kawaida, kufanya tafiti mbali mbali ni miongoni mwa majukumu ya msingi ya vyuo vikuu, jambo ambalo hutoa mchango wa chuo kitaaluma na kupandisha hadhi ya ubora wa chuo chenyewe. Chuo chetu hiki kina dhima kubwa ya kutoa taaluma bora inayoambatana na kufanya tafiti kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizomo katika jamii yetu. Nakuhimizeni sana muendelee kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania (COSTECH), ambayo ina wajibu wa kuwawezesha watafiti mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar kufanya tafiti wanazozikusudia.

Kadhalika, mna wajibu wa kutafuta fedha za kufanya tafiti kutoka vyanzo mbali mbali kwani utafiti ni miongoni mwa majukumu yenu. Hakuna maendeleo bila ya utafiti. Vile vile, natambua kuwa utafiti ni ngazi muhimu ya Wanachuo wetu wa mafunzo ya Uzamili na Uzamivu, ili waweza kuhitimu masomo yao.

Jambo jengine ninalotaka nilihimize ni haja ya kuendeleza masuala ya michezo na uendelezaji wa midahalo. Masuala haya ni muhimu katika vyuo kwa lengo la kuimarisha afya za wanachuo na kuwaongezea maarifa ya masuala mbali mbali ya kitaaluma. Michezo inachangia sana katika kuimarisha afya na kuchangamsha akili ya mwanafunzi. Vile vile, michezo hujenga uhusiano mzuri wa jamii na watu kujuana na kufahamiana. Kadhalika, vilabu vya wanafunzi huchangia katika kuongeza ushindani miongoni mwa wanafunzi katika masuala mbali mbali na kuibua vipaji. Kwa bahati mbaya, katika taarifa zote zilizotangulia kutolewa hapa, suala la michezo limesahauliwa kuelezewa na kupewa umuhimu wake unaostahiki.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Kabla ya sijamaliza hotuba yangu, napenda kuwaasa wanachuo wanaoendelea na masomo yao hapa Chuoni kufanya bidii, ili na wao wapate matokeo mazuri yatakayowawezesha kufikia ndoto zao za kimaisha. Kumbukeni ule usemi maarufu uliosemwa na aliyekuwa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Marehemu Nelson Mandela, usemao: nanukuu

“Education is the most powerful weapon which you can use to change the

world” Mwisho wa kunukuu. Tafsiri:

„Elimu ndio silaha yenye nguvu zaidi duniani ambayo mtu anaweza kuitumia katika kuleta mabadiliko‟.

Kwa msingi huo, ili tuweze kuyabadili maisha yenu, ili yaendane na ndoto zenu pamoja na mipango ya nchi yetu, lazima mjitahidi katika kutafuta elimu. Vile vile, kila wakati zingatieni maneno ya hekima ya Rais wa Mwanzo wa Zanzibar,Marehemu Mzee Abeid Amani Karume yasemayo; “Jifunze wakati ndio huu”. Kwahivyo, na nyinyi utumieni vizuri muda huu wa kuwepo hapa chuoni, kwa ajili ya kusoma zaidi na kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kukuharibieni masomo yenu na maisha yenu.

Tumieni vizuri Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa mambo yenye manufaa na yatakayokusaidieni kuongeza taaluma yenu. Jitayarisheni vizuri na mitihani yenu, na kamwe msijenge utamaduni wa kukopia, kufanyiwa kazi zenu na kushughulika na mitihani iliyovuja. Mambo yote haya, yanaathiri hadhi na thamani ya mfumo wetu wa elimu, ubora wa vyuo vyetu ambavyo tunaendelea kutumia fedha nyingi na juhudi kubwa katika kuviimarisha pamoja na kuathiri fursa za kupata ajira pale mnapotafuta kazi. Kadhalika, nakuhimizeni kwamba kila aliyehitimu leo, ahakikishe ana mipango imara na thabiti ya kujiendeleza kwa kuzingatia hekima yakwamba „Elimu haina mwisho‟.

Nakuhimizeni wahitimu mliokwishaajiriwa kwamba mwende mkaoneshe tafauti katika utekelezaji wa majukumu yenu mtakaporudi sehemu zenu za kazi. Jambo hili litasaidia kubainisha kuwa, maarifa mliyoyapata wakati mkiwa chuoni, yameweza kukusaidieni kuongeza ufanisi katika kufanya kazi zenu. Aidha, na nyinyi ambao hamjaajiriwa, pindi mkiajiriwa, ni vyema mkathibitisha uwezo wenu wa kufanyakazi vizuri kutokana na maarifa mliyoyapata hapa chuoni.

Kwa kuwa si rahisi, wahitimu wote kupata ajira Serikalini, nakuhimizeni kuzichangamkia fursa zilizoandaliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi na mipango mingine, ili muweze kujiari wenyewe. Leo si siku ya kusema mengi kuhusu mpango wa Serikali wa kuwawezesha wananchi kiuchumi. Katika siku za hivi karibuni tutatangaza mipango yetu ya ziada. Hata hivyo. leo, nawahimiza wale wote wenye dhamira ya kujiajiri wenyewe wajipange vizuri mambo mazuri yanakuja. Kuweni na ndoto kubwa zaidi ya kujiajiri kuliko kutaka kuajiriwa Serikalini, mkitambua kwamba matajiri na watu maarufu zaidi duniani, wengi wao ni watu waliojiajiri wenyewe kwa kujishughulisha na biashara, sanaa, michezo na shughuli mbali mbali za ujasiriamali. Nanyi mkiamua mnaweza kuwa miongoni mwa watu hao.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Serikali imo katika kukamilisha taratibu zitakazotuwezesha kuwa na fedha za kutosha za kuwawezesha wananchi kiuchumi. Nina furaha kuona kwamba tayari wapo baadhi ya wahitimu wasomi ambao wamezitumia vyema fursa zilizokuwepo kupitia mfuko wa Uwezeshaji kwa kuendesha maisha yao bila ya kuajiriwa Serikalini.

Kwa upande mwengine, nakuhimizeni kwamba mara tu mtakapopata ajira, muendeleze uaminifu na uadilifu mlionao kwa kulipa mikopo ya masomo kwa wale ambao walikopa na kukopeshwa mikopo hiyo.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo na Wageni Waalikwa,

Namalizia hotuba yangu kwa kukupongezeni nyote kwa kufanikisha sherehe za Mahafali ya Kumi na Nne ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa mafanikio makubwa. Kwa hakika sherehe hizi za mahafali zimefana sana.Tunaipongeza sana kamati ya maandalizi kwa kazi nzuri waliyoifanya. Natoa shukurani maalumu kwa uongozi, wahadhiri na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, kwa jitihada zenu na ushirikiano mkubwa mnaonipa nikiwa Mkuu wa Chuo hiki. Ushirikiano wa kila mmoja wetu, mapenzi, uwajibikaji na uzalendo ndio siri kubwa ya mafanikio tunayoendelea kuyapata. Nasaha zangu kwenu, ni kuwa tuudumishe mwendo huu na tuongeze kasi katika utekelezaji wa majukumu yetu, ili Chuo hiki kiendelee kuwa chemu chemu ya kutoa wasomi mahiri na waliobobea wenye maarifa na moyo wa uzalendo katika kuitumikia nchi yetu na kuimarisha ustawi wa maisha ya jamii yetu.

Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe nguvu na uwezo zaidi wa kuyatekeleza kwa ufanisi malengo yote tuliyojipangia katika kuimarisha maendeleo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Atuzidishie amani, umoja na mshikamano. Mola wetu atupe elimu na utambuzi wa kuweza kuzitumia vyema rasilimali zote alizotujaaliwa hapa nchini, ili zilete manufaa kwa kizazi cha sasa na wale watakao kuja baada yetu. Namuomba Mwenyezi Mungu aturudishe sote nyumbani kwa salama.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.