SUZA yadhamini mafunzo watayarishaji wa vipindi
Na Nasima Haji, MWANZA
CHUO Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimepokeza cheti cha Shukurani kufuatia kudhamini mkutano wa mafunzo wa 108 wa watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma yaliyotolewa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Cheti hicho kimetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye kutokana na kuthamini mchango na ushiriki wa maofisa waliopata mafunzo hayo walioziwakilisha taasisi zao kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao pia wamechangia mkutano huo.
Katika mafunzo hayo, maofisa wa habari zaidi ya 120 kutoka taasisi za serikali, mashirika ya umma na binafsi ulifayika leo katika hoteli ya Crest, jijini Mwanza.
Washiriki walijifunza mada kadhaa zikiwemo, mawasiliano ya ushawishi, mawasiliano ya kimkakati, uzalendo katika muktadha wa dhana nne za uvumilivu (Reconciliation), ustahamilivu (Resilience), Ukarabati (Rebuilding), na mageuzi (Reform). Mada nyengine ni matumizi ya mitandao, utayarishaji wa vipindi vya televisheni na redio na upigaji picha.
Akiwahutubia washiriki wa mafunzo hayo, Mhe. Nnauye aliwahimiza maofisa wa mawasiliano na uhusiano kupitia kwenye taasisi zao kutumia vyombo vya habari kupeleka maudhui yenye mtazamo chanya ambao utaleta mabadiliko kwa jamii.
Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina jukumu ya kutoa maoni ya wananchi ili taasisi zinazohusika ziweze kuyachukua na kuyafanyia kazi.
‘’ Ni matumaini yangu kuwa mkutano huu utaandaa vipindi na taarifa zinazolenga kutatua kero za wananchi’, alisisitiza.
Mkutano huo wa siku tano ambao ulianza jana na kumalizika siku ya Ijumaa wiki hii na utawawezesha washiriki hao kutembelea maeneo ya vivutio, historia na miradi ya mikakati.