SUZA wapewa jukumu kupitia sheria za bahari
Na Nasima Haji, SUZA
Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi, Kepteni Abdallah Hussein Kombo, ameuagiza uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kushirikiana na wadau kupitia sheria za matumizi bora ya bahari ili kufikia malengo na vigezo vya kimataifa.
Akizungumza katika kikao cha mradi wa kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika katika soko la uchumi wa buluu Zanzibar (Skills Development for Youth Employability in the Blue Economy– SEBEP), kilichofanyika huko Maruhubi mwishoni mwa wiki.
Alisema sheria hizo hazikidhi haja kwa sababu sera ya matumizi ya bahari tayari imebadilishwa na kwamba iko haja ya sheria kuendana na matakwa ya matumizi ya bahari yanayotakiwa hivi sasa.
‘’ Jitihada mbali mbali zilifanyika kubadilisha sheria lakini hazikufanikiwa, sasa hili ni suala la nyinyi SUZA kuwaita wadau kuijadili, kutoa maoni yao ili kutengeneza mchakato wa kuona wapi tunataka kwenda’’ , alisisitiza
Kuhusu matumizi ya bahari, alihimiza kuwepo mtaala maalum wa kuielimisha jamii namna bora ya kuitumia kwa ajili ya kuwawezesha watu wengi zaidi kufaidika na hazina hiyo.
Akizungumzia kuhusiana na uhifadhi wa mazingira alikumbusha kuwa kuna umuhimu wa kuweka kikosi cha kuangalia usafi wa mazingira hasa ikizingatiwa kuwa zipo taasisi nyingi zinazohusika kuangalia ustawi wa matumizi bora ya bahari na rasilimali zake.`
Mapema, Makamu Mkuu wa SUZA, Profesa Moh’d Makame Haji, wakati akimkaribisha mgeni rasmi wa warsha hiyo alisema SUZA kimepewa jukumu na uongozi wa awamu ya nane unaoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuongeza nguvu katika ustawi wa uchumi wa buluu, kuvuna bidhaa za bahari ikiwa ni pamoja na kuvuna mazao ya bahari na kudumisha uhusiano baina ya pande mbili.
’’ Mradi huu wa SEBEP unatupa fursa na nguvu ya kuhakikisha kuwa tunaweza kuyafikia malengo yetu.
Miongoni mwa malengo hayo ni kuimarisha ubora na ufanisi wa upatikanaji wa taaluma, kuongeza kiwango cha ajira kwa vijana kwa kutumia rasilimali zake za Zanzibar za asili, kuimarisha taaluma ya ujasiriamali
Akiwasilisha mada kuhusu kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika katika soko la Uchumi wa Buluu Zanzibar, Mratibu wa mradi huo kutoka SUZA, Dkt. Yahya Hamad Sheikh, alisema mradi huo utachangia kupunguza ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira Zanzibar.
Akitoa takwimu za mtiririko wa vijana wasiokuwa na ajira mwaka mwaka 2006 lilikuwa 379,038 hadi kufikia 568,094 mwaka 2021 ambao ni vijana wenye umri wa miaka 15 -35 imeongezeka kutoka asilimia 19.6 (2006) hadi asilimia 27.4 (2021). Huku vijana wanawake wasiokuwa na ajira inakadiriwa kufikia asilimia 40.6 kwa mwaka (2021) kutoka asilimia 15.4 (2006).
‘’ Serikali inalenga kuwapatia vijana ujuzi unaokubalika katika soko la ajira linaloweza kuwapatia ajira wakiwa wameajiriwa au kujiajiri’’, alisema.
Naye Raya Juma Khalfan, mwakilishi kutoka jumuia ya wanawake mabaharia alishauri kuwepo Chuo kitakachowafundisha mabaharia wanawake kwani wamekuwa wakishindwa kujipatia elimu nje ya Zanzibar kutokana na gharama kubwa za masomo ya ubaharia na usafiri nje ya Zanzibar.
‘’Wanawake wengi wanavutiwa na kusoma ubaharia lakini wanashindwa kutokana na gharama za mafunzo, yakitolewa hapa Zanzibar yatasaidia’’, alisema.
Khamis Rashid ambaye ana uzoefu katika masuala ya ubaharia alisema kwa masikitiko kuwa asilimia 80 ya mabaharia wa Zanzibar ni kutoka Tanzania bara ambapo Zanzibar imeshawaandaa vijana wengi mabaharia ambao hawatumiki.
‘Cheti hakitoshi, uzoefu ni muhimu na wenye uzoefu wapo tuwatafute, hatuwatumii na mwisho wake watatukimbia,’’ alisema baharia mzoefu, Khamis Rashid.
Aidha, alipendekeza kuwa ni vyema taasisi inayosimamia ustawi wa masuala ya baharini ikatafuta vifaa kwani wataalamu wapo wa kutosha ambao wamekuwa wakitumika endapo zinatokea kazi za dharura kwenye meli.
Mradi wa huu unaotarajiwa kugharimu shilingi 125b utagharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa asilimia 90 na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia 10 umeanza utekelezaji wake mwezi Mei mwaka jana na kukamilika mwezi Septemba mwaka 2027.
mwisho